RAIS John Pombe Magufuli na Rais Abdel Fattah Al Sisi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri wameahidi kuongeza nguvu katika kuimarisha na kuendeleza uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi zao.
Wakizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar Es Salaam mara baada ya kuongoza mkutano wa mashauriano kati ya Serikali za Tanzania na Misri, viongozi hao walisema kuwa katika mkutano huo pande mbili hizo zimekubaliana kuchukua hatua za haraka ili kuongeza kasi ya uhusiano na ushirikiano.
“Tumekubaliana kuongeza kasi ya uhusiano na ushirikiano wetu na katika kutekeleza hilo tumeamua kufufua Kamisheni ya Ushirikiano kati ya nchi zetu na kuagiza mikutano hiyo ya mashaurisno ifanyike kwa haraka”Rais Magufuli alieleza.
Alieleza kuwa Kamisheni hiyo ambayo ndio inayoratibu na kuongoza mashirikiano kati ya nchi hizo ilikutana kwa mara ya mwishio miaka 20 iliyopita hivyo kupunguza kasi ya mashirikiano katika baadhi ya maeneo.
Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Serikali hizo nimedhamiria kuimarisha uhusiano kati yao ikiwa ni sehemu ya kuienzi historia nzuri ya ushirikiano iliyoasisiwa na Rais Julius Nyerere na Gamal Abdel Nasser.
Katika mnasaba huo, nchi hizo zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika maeneo yanayoshirikiana sasa na kuangalia maeneo mengine zaidi kwa manufaa ya Serikali na wananchi wa pande zote mbili.
Rais Magufuli aliyataja mambo mengine waliyokubaliana kuwa ni pamoja na kupanua biashara na uwekezaji, kilimo, elimu, afya pamoja na ulinzi na usalama.
Alibanisha kuwa chini ya makubaliano hayo, Misri itaanzisha kiwanda kikubwa na kisasa cha nyama humu nchini ili nchi hiyo iweze kukidhi mahitaji yake ya nyama pamoja na kuuza katika masoko ya nje.
Halikadhalika, Misri imeahidi kupanua wigo wa misaada yake kwa Tanzania katika sekta za afya na elimu ambapo kwa upande wa afya nchi hiyo itaijengea uwezo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili iweze kufanya upasuaji wa figo ifikapo mwaka 2020.
Kwa upande wa elimu, Rais Magufuli alibainisha kuwa nchi hiyo imekubali kuongeza nafasi za masomo kwa vijana wa Tanzania ambapo alieleza kuwa kwa sasa watanzania 115 wako nchini humo wakichukua mafunzo katika fani mbali mbali.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO