Na Mwandishi Wetu- MAELEZO, Dodoma
Heshima na hadhi ya Tanzania Kimataifa imeendelea kupanda kutokana na nia njema na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo (Agosti 31, 2019) Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa Serikali kwa mwezi Agosti 2019.
Dkt. Abaasi anasema: “kwa mujibu wa Ripoti iliyotolewa Julai 12, 2019 kwa pamoja kati ya Transparency International na Afro-Barometer, Tanzania imeongoza katika nchi 35 kwa kuonesha juhudi za wazi katika kupambana na rushwa”.
“Mafanikio haya yanatokana na msimamo thabiti wa Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake katika kuimarisha taasisi muhimu kama vile TAKUKURU, Kuanzisha Mahakama ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi, mfumo wa udhibiti wa rushwa katika manunuzi kupitia PPRA”, ameongeza Dkt. Abbasi.
Akitolea mfano, amesema kuwa TAKUKURU imeokoa jumla ya shilingi bilioni 86 zilizotokana na mishahara hewa na ukwepaji kodi.
Aidha, Dkt Abbasi ameabainisha kuwa jumla ya shilingi bilioni 25.5 zimerejeshwa Serikalini kwa mchanganuo ufuatao; bilioni 14.6 ikiwa ni urejeshwaji wa mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu na bilioni 10.9 zilizotokana na thamani ya mali zilizotaifishwa yakiwemo magari, vituo vya mafuta, nyumba nane, magari nane na Bilioni 20 ambazo ni mali zilizozuiwa kesi zikiendelea.
Amesema kuwa kwa upande wa Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imeokoa takribani shilingi bilioni 46.9 zilizokuwa zipotee kutokana na kutofuatwa taratibu za ununuzi, malipo ya zaidi ya mkataba kwa wakandarasi au baadhi kutorudisha fedha walizopewa kama dhamana na uzembe na rushwa.
Akizungumzia utekelezaji katika sekta ya uchukuzi, Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali imeanza zabuni ya kuagiza vichwa 22 (vitano vya mafuta yaani Diesel Locomotive na 17 vya umeme yaani Electrical Locomotive) na mabehewa ya abiria 60 na 1430 ya mizigo.
Aidha ameongeza kuwa, Serikali imeanza zabuni ya treni tano (5) zilizokamilika (Electrical Multiple Unit) za abiria zenye mabehewa nane (8) kila moja na vichwa viwili kwa ajili ya uendeshaji wa treni za abiria kwa kipande cha Dar es salaam hadi Morogoro na kisha Dodoma
Mbali na hayo, ameeleza kuwa, Serikali imetenga fedha za ndani shilingi Bilioni 71.4 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja jipya la Mto Wami lenye urefu wa Mita 513.5 litakalojumuisha ujenzi wa barabara za KM 4.3 kwa kila upande ambapo kazi ya ujenzi huo imeshaanza.
Pia, Serikali imesaini mkataba wa shilingi bilioni 699.9 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja refu zaidi Afrika Mashariki na Kati la Kilometa 3.2 kuunganisha mikoa ya Mwanza na Geita kwenye eneo la Kigongo-Busisi katika Ziwa Victoria.
Katika Sekta ya Afya, Dkt Abbasi amesema kuwa, Serikali imeshatoa shilingi bilioni 30 kwa ajili ya Ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa (RHH) na sehemu nyingi ujenzi umekamilika. Mikoa husika ni; Mwanza, Simiyu, Njombe, Songwe, Katavi, Geita na Dar es Salaam (Mwananyamala) na kuna Bilioni 3 imetolewa Kujenga Hospitali ya Kanda ya Wazazi Mbeya na shilingi bilioni 6.32 kujenga Hospitali ya Kanda Mtwara.
Vilevile, katika kuwekeza katika maisha ya watu ngazi ya Wilaya, Serikali mapema mwaka huu ilitoa shilingi Bilioni 105 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya 67 ambapo katika miaka zaidi ya 50 ya Uhuru tumekuwa na Hospitali katika Wilaya 77 tu; ndani ya mwaka huu mmoja zinajengwa 67 ambapo ujenzi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
“Niwathibitishie Watanzania kuwa azma yetu ya kuiendeleza nchi kwa kasi chini ya Jemedari Dkt. John Pombe Magufuli inaendelea kushika kasi na katika hili hakuna mwanadamu wa kutuzuia wala kuturudisha nyuma” Amesisitiza Dkt Abbasi.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO